ZACADIA YATOA MSAADA WA VITABU KWA TAASISI ZA ELIMU ZANZIBAR

  • Aug 06, 2018
  • 169 Views

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Diaspora Zanzibar Ndugu Adila Hilal Vuai ameendelea kuwashajihisha Wazanzibari wanaoishi Nchi za Nje kuitikia wito wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein wa kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.

Ndugu Adila ameyaeleza hayo wakati alipokuwa akikabidhi msaada wa vitabu vya aina mbalimbali kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar vyenye thamani ya shilingi 1,465,380,000/= vilivyotolewa na Jumuiya ya Wazanzibari wanaoishi nchini Canada (Zanzibar Canadian Diaspora - ZACADIA). Amesema Serikali inathamini sana misaada inayotolewa na wanadiaspora na ndio maana tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar, mapema mwezi Mei mwaka 2018 imezinduwa Sera ya Diaspora ya Zanzibar ambayo inafafanua misingi ya kufaidika na michango ya Wanadiaspora wa Zanzibar kwa maendeleo ya Zanzibar kiuchumi na kijamii, wakati huo huo inaweka wazi mahitaji yao kwa kuweka utaratibu mzuri utakaosaidia kujenga uaminifu na kuwavutia Wanadiaspora hao kuimarisha mahusiano na Nchi yao ya asili.

Sera hii inajumuisha mambo muhimu na hatua mahsusi pamoja na mahitaji ya mfumo wa Sheria na Taasisi ambao utawekwa kuondosha changamoto zilizopo ili kuweza kuwashirikisha kikamilifu Wanadiaspora wa Zanzibar katika maendeleo ya nchi yao.Akipokea vitabu hivyo kwa niaba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mkurugenzi wa Elimu Sekondari Bi Asia Idd Issa amewataka wawakilishi wa taasisi za elimu zilizopokea msaada huo kuwa makini katika matumizi na kuvitunza vitabu hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kuwanufaisha zaidi. Aidha, Mkurugenzi huyo, aliwaelekeza waalimu kuwahimiza wanafunzi kuvitunza na kuvitumia ipasavyo vitabu hivyo na kujenga utamaduni wa kujisomea utakaoleta matokeo mazuri ya mitihani yao.

Nae, meneja wa ZACADIA kanda ya Unguja Bi Firdaus Rashid Rabia ameahidi kuwa ZACADIA itaendelea kutoa misaada yenye manufaa makubwa kwa jamii lakini pia ameziomba taasisi hizo kuthamini nguvu na jitihada za wanadiaspora hao ili kuwatia shime ya kuongeza juhudi zao.

Akitoa shukurani zake, kwa niaba ya taasisi za elimu za Zanzibar zilizopokea vitabu hivyo, ndugu Maalim Hamad Mkubwa kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, ameahidi kufuata ushauri uliyotolewa juu ya kuvitunza na kuvitumia ipasavyo vitabu hivyo ili kufikia lengo lililokusudiwa. Miongoni mwa taasisi zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST), Chuo cha Kilimo Kizimbani na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA).

Related Articles