WANADIASPORA WA ZANZIBAR WAPONGEZWA KILA KONA

  • Aug 01, 2016
  • 155 Views

Masheha wa Wilaya ya Mjini pamoja na wananchi kutoka vijji mbali mbali na taasisi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Unguja na Pemba wamewapongeza na kuwashukuru Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kwa kuitikia wito wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Jumuia zao wakiwa nje ya Zanzibar kwa lengo la kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti siku chache baada ya kumalizika kwa semina iliyotayarishwa na Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi iliyolenga kutoa elimu ya mtangamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki na Diaspora na kuwashirikisha masheha wa Wilaya ya mjini iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari Kikwajuni baadhi ya taasisi za serikali, masheha wa Wilaya ya mjini pamoja na wananchi wa sehemu mbali mbali wa mjini na vijiji Unguja na Pemba wameelezea kuridhishwa kwao kwa kuwepo kwa kitengo cha Diaspora kwa kupongeza na kuzishukuru jumuia ambazo zimeshaanza kutoa misaada kwa jamii.

Sheha wa Shehia ya Mpendae Wilaya ya mjini Bw. Haji Seti Haji aliwapongeza Wazanzibari walioko nchi za nje kwa kuitikia wito wa serikali wa kuanzisha jumuia zao na kuanza kazi zao kwa kutoa misaada mbali mbali kwa jamii ya wazanzibari hali ambayo inastahili kuungwa mkono na kupongezwa na kila mzanzibari anaependa maendeleo ya nchi yetu. 

`Wameanza vizuri ndugu zetu walioko nchi za nje katika kuisiaidia jamii lakini ninachowataharidha wenzetu walenge walichokikusudia na wala wasije wakajiingiza na mitego ya wana siasa kwani wanaweza kuzivunjia hadhi jumuia zao ambazo hivi sasa wananchi wanaziamini vilivyo.

Nae Sheha wa Shehia ya Kikwajuni Juu Bibi Asha Ali Ali Ameipongeza Idara inayohusiana na Diaspora Zanzibar kwa kuwapatia semina muhimu ambayo wameweza kujifunza mambo mengi ya kupata mwanga na elimu ya kutosha juu ya ndugu zao walioko nje ya nchi na faida zao na maendeleo ya nchi zao. `Mimi hadi nilikuwa nafika katika ukumbi ule wa semina ya Diaspora kwa Masheha nilikuwa sijui kiundani hasa maana ya Diaspora na faida zake lakini sasa naunga mkono kuwepo kwao na sisi masheha tutakuwa kila mstari wa mbele kushirikiana nao wanapokuwa wanahitaji misaada kutoka kutoka kwetu` alisema Sheha huyo wa Shehia ya Kikwajuni Juu.

Nae Sheha wa Shehia ya Mto pepo Bw. Hassan Masoud Hassan amesema ingawa Wilaya yake ya Maghribi haikushiriki katika semina hiyo Bw. Hassan amezipongeza jumuia hizo za Diaspora kwa utaratibu wao wa kusaidia hasa familia masikini na watoto mayatima. `Mimi ninapongeza kidhabiti wana Diaspora hao na hasa Jumua ya Wazanzibari wanaoishi nchini Canada ZACADIA kwa kuwa na utaratibu wa kuzisadia familia masikini na watoto mayatima kila inapofika wakati wa mwezi mtuufu wa Ramadhani na nawaombee Mungu waendelee na utaratibu huo` alisema Sheha huyo.

Bibi Mwanavisi Hassan wa Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja amewapongeza Wanadiaspora walisaidia huduma za afya katika kituo cha Cottage cha Makunduchi ambacho hivi sasa kinatoa huduma za afya vizuri katika kiwango kinachokubalika kutokana na michango yao ya vifaa na madawa. `Tunawaombea dua ndugu zetu walioko nje Mwenyezi Mungu awazidishie baraka ili waendelee na moyo wao wa kizisaidia sekta za huduma muhimu hasa za afya, maji na elimu` alisema.

Nao walimu na wanafunzi wa skuli ya Unguja Ukuu Wilaya ya Kati wameupongeza Umoja wa wazanzibari wanaoishi nchini Canada Zanzibar Help Foundation kwa kuwapatiawalimu wa kujitolea kutoka nje ya nchi kwa kusomesha sayansi na lugha ya kiingereza pamoja na kuyafanyia ukarabati baadhi ya majengo ya skuli hiyo ambayo hivi sasa yanaonekana katika mazingira bora zaidi.

Wizara ya elimu na mafunzo ya amali kwa upande wake imekuwa ikitoa pongezamara kwa mara wa jumuia hizo ukiwemo Umoja wa Wazanzibari wanaoishi nchini Marekani, Umoja wa Wazanzibari wanaoishi Dubai UAE( Milele Foundation kwa Misaada yao   ikiwemo ya vitabu, compyuta na Laptop, ujenzi wa madarasa,viti, meza, vifaa vya maabara kwa ajili ya kusambazwa katika skuli zenye mahitaji hayo.

Katika sekta ambayo nayo imekuwa ikitolewa pongezi za jumla kwa serikali na wananchi ni sekta ya afya ambayo wazanzibari walioko nchi mbali mbali wamekuwa wakielekeza misaada yao katika sekta hiyo. 

Miongoni mwa misaada hiyo ni ukarabati wa hospitali ya zamani ya kijiji cha Mahonda na kutoa huduma bora za afya pamoja na vifaa vya kisasa katika hospitali hiyo kumefanywa na Mwanadiaspora kutoka nchini Marekani DR. Ameesh Mehta. 

Vilele kumetolewa Vifaa vya afya katika Hospitali ya Mikunguni vilivyotolewa na Jumuia ya Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza (ZAWA). Nacho kituo cha afya cha Kengeja kilichoko Wilaya ya Mkoani kimepatiwa vifaa vya afya vilivyotolewa na Jumuia ya Wazanzibari wanaoishi nchini Canada(ZACADIA)

Pamoja na kasi hiyo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuona jumuia hizo zinaendelea kuimarika na kuwepo inaendelea na itihada zake za kuwaandalia mazingira mazuri zaidi wanadiaspora hao ikiwemo hatua ya kuanadaa sera maalum itakayozilinda jumuia hizo wakiwa nje na ndani.

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa wazanzibari wanaoishi nchi za nje nd. Adila Hilal Vuai amesema idara yake itaendelea kutoa elimu zaidi dhana Zanzibar na Diaspora na maendeleo ili kila mmoja wetu afahamu vilivyo umuhimu wa Diaspora na maendeleo yake kiuchui na kijamii.

Related Articles