SMZ yaandaa sera ya diaspora kuvutia walio nje

  • Mar 21, 2014
  • 137 Views

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema tayari imeweka mazingira mazuri ambayo yatasaidia Wazanzibari waliopo nje ya nchi kuwekeza Zanzibar na kusaidia katika miradi mbalimbali. Hayo yalisemwa na Mshauri wa Rais anayeshughulikia vitega uchumi na uwekezaji Balozi Mohamed Ramia wakati akifungua mkutano uliowashirikisha Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi.

Alisema tayari Serikali ipo katika mchakato wa kutayarisha Sera ya Diaspora ambayo itakuwa muongozo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema tangu kuanzishwa kwa Idara ya Diaspora mara baada ya Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein alipoingia madarakani mwaka 2010, Idara hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuwashawishi wananchi wengi wenye asili ya Zanzibar kusaidia maendeleo ya nchi.

Mkurugenzi wa diaspora Khamis Mohamed alisema matayarisho ya Sera ya Diaspora ipo katika hatua za mwisho kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi mjini hapa.

Alisema sera hiyo itasaidia kuweka mazingira mazuri ambayo Wazanzibari waliopo nje watakuwa na fursa na nafasi nzuri ya kutoa mchango wake kwa taifa.

Mzanzibari anayeishi nchini Sweden, Mohamed Saleh alisema kuwepo kwa sera kutakuwa chachu ya kuleta maendeleo na wananchi kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa mfano alisema Wazanzibari waliopo nje wanahitaji kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari ambavyo vitatoa nafasi kama utambulisho wa kushiriki maendeleo ya Zanzibar.

“Sisi Wazanzibari tuliopo nje ya nchi tunahitaji kutambuliwa rasmi ikiwemo kupata kitambulisho cha Mzanzibari mkazi ambacho kitatupa nafasi ya kushiriki maendeleo ya taifa,” alisema.
Idara ya Diaspora tayari imefanya ziara zaidi ya nchi tano kwa ajili ya kuwasiliana na Wazanzibari waliopo nje ya nchi kusaidia maendeleo ya taifa.

Source: Khatibu Suleiman - Habari Leo

Related Articles