Ilikuwa ni tukio la aina yake, wakati Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein alipokutana na Wazanzibari wanaoishi nchi za nje katika hafla ya Chakula cha mchana aliyoiandaa kwa ajili yao katika Viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar tarehe 9/08/2014. Katika hafla hio vile vile alihudhuria Makamo wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.
Wazanzibari kutoka Uingeraza, Nchi za Nordia,Marekani,Canada, Australia,Switzerland,Oman,UAE,Ujerumani, walikuwepo katika Hafla hio.Akiongea na hadhara iliyojumuisha Diaspora hao, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein alionyeshwa kufurahishwa kwake kwa Diaspora hao kuitikia kwa wingi mualiko wake, lakini pia kwa kuonesha upendo na uzalendo kwa nchi yao kwa kuekeza na kuchangia katika sekta za elimu na afya.
Vile vile Mheshimiwa Rais, alitumia fursa hio kuwashauri Wazanzibari na Watanzania wanaoishi nchi za nje, kutosahau kwao na wajitahidi kujiwekea Khatma ya baadae kama vile kujenga nyumba, badala ya kukaa katika mahoteli kila wanapokuja Zanzibar.
Aidha, Mheshimiwa Rais aligusia suala la kudumisha utamaduni wa Kizanzibari kwa vizazi vinavyozaliwa nchi za nje ili vijuwe asili yao na kuendeleza utamaduni wa nchi yao.
Akitoa neno la shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mwakilishi wa Wazanzibari wanaoishi nchi za nje Nd. Hafsa Mbamba alimshukuru Rais wa Zanzibar na kumtakia kila la kheri kwa upendo wake anaouonesha kwa Wazanzibari wanaoishi nchi za nje. Nd. Hafsa alimhakikishia Mheshimiwa Rais, Kuwa wote waliohudhuria hafla hii watakuwa Mabalozi wazuri katika kuitangaza Zanzibar katika nchi za nje, na kuwahamasisha wale ambao hawakushiriki katika hafla hio, kufanya hivyo katika kipindi kijacho.
Na mwisho hadhara hio ilipata fursa ya kumsalimia Mheshimiwa Rais kwa kupeana mikono na kupiga nae picha.