Wasifu wa Marehemu Khamis Ali Khamis

  • Sep 19, 2014
  • 169 Views
Khamis Ali Khamis

Marehemu Khamis Ali Khamis alizaliwa tarehe 28 Oktoba, 1962 Zanzibar. Alianza elimu yake ya msingi mwaka 1969 na kumalizia elimu ya Sekondari hapa hapa Zanzibar mwaka 1983. Katika mwaka 1986 alianza masomo ya Stashahada ya lugha katika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni kabla ya kuanza masomo shahada ya kwanza ya Sayansi ya Uchumi nchini Yugoslavia mwaka 1986 hadi mwaka 1993, ambako alifaulu na kutunukiwa shahada hiyo.
 

Mwaka 1996 hadi mwaka 1997 alifanya stashahada ya uzamili ya Mipango ya Maendeleo Vijijini nchini India. Aidha, alihudhuria masomo mafupi ya fani mbali mbali ndani na nje ya nchi kama vile ushirikiano wa kimataifa, sera kuhusiana na masuala ya uongozi, uchumi na utafiti na nyengine nyingi.

Alianza kuwa mtumishi wa umma mwaka 1985 alipoajiriwa na Wizara ya Biashara, Viwanda na Utalii katika hoteli ya Bawani akiwa kama mpokezi wa wageni.Mnamo mwaka 1993 hadi mwaka 1994 alikuwa afisa wa mapato katika Kamisheni ya Utalii ambapo baadae mwaka huo aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mipango katika Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uchumi Zanzibar.

Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa msaidizi Mwandishi wa Hotuba za Rais katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Mawasiliano na habari Ikulu Zanzibar hadi mwaka 2011 alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Wazanzibari Waliopo Nje wadhifa ambao aliendelea nao hadi kufariki kwake.

Katika kipindi chote cha utumishi wake, marehemu alikuwa mchapa kazi hodari mwenye kufanyakazi kwa mashirikiano makubwa na wenzake wote.Wakati wote hakusita kutaka ushauri kutoka kwa wafanyakazi wenzake katika ngazi ya chini, waliyo kwenye kada moja na vile vile viongozi wake. Marehemu Khamis Ali Khamis ataendelea kukumbukwa kutokana na ubunifu wake katika kazi, mashirikiano na wenzake na kuwa mkurugenzi wa kwanza kuiongoza Idara ya Uratibu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Wazanzibari Waliopo Nje.

Marehemu ameacha vizuka wawili na watoto wanne.Tumuombe Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi.

Kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, tunawapa pole wafiwa wote. Mwenyezi Mungu awajaalie subira na sote atupe khatma njema.

Inna Lillah wa inna ilayhi rajiun.
Ahsanteni

Related Articles