Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2001, toleo jipya la mwaka 2024, ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na ni nyenzo madhubuti ya kulinda na kutetea maslahi ya taifa ndani na nje ya mipaka.
Aidha, amesema kuwa Sera hiyo inalenga kufungua milango ya fursa mpya za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa pande zote za Muungano, hususan Zanzibar, ambayo kwa kiwango kikubwa inategemea sekta ya nje kwa maendeleo yake. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa Sera mpya uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), leo tarehe 19 Mei 2025, Jijini Dar es Salaam.
Vilevile, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusimama imara maboresho ya Sera hiyo, pamoja na hatua kubwa zilizochukuliwa za kuimarisha diplomasia. Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa sekta ya utalii, usafirishaji wa baharini, uzalishaji wa bidhaa kama mwani na karafuu, pamoja na uwekezaji wa miradi ya maendeleo, ni mifano ya utegemezi mkubwa wa Zanzibar katika diplomasia ya kiuchumi.
Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi ameihimiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha inashawishi mataifa rafiki kuanzisha ofisi za uwakilishi Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wageni. Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia pia kukuza uwekezaji, kuimarisha sekta ya utalii, na kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara.