Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii, Mhe. Masoud Ali Mohammed, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mpango wa kuandaa jukwaa la Diaspora litakalowawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuleta maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza leo, tarehe 2 Novemba 2026, katika kikao cha kujadili maendeleo ya Diaspora kilichofanyika Ikulu, Waziri Masoud amesema jukwaa hilo litakuwa fursa muhimu ya kusikiliza changamoto zinazowakabili Watanzania hao, kubadilishana mawazo na kujadili namna bora ya kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na Serikali.
Amesema jukwaa hilo pia litatoa nafasi kwa Diaspora kuwasilisha maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha ushiriki wao katika mipango na mikakati ya maendeleo ya Zanzibar. Aidha, amewataka Diaspora waliopo Zanzibar kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao wanaoishi nje ya nchi kwa kuitangaza Zanzibar na kueleza fursa mbalimbali zilizopo, zikiwemo miradi ya maendeleo na maeneo ya uwekezaji.
Waziri Masoud amewahimiza pia kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu na ujuzi kwa vijana, ili kuwawezesha kutumia maarifa waliyonayo katika kujiajiri, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kujiletea maendeleo. Akizungumzia suala la uwekezaji, amewataka Diaspora kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi kwani ujuzi na uzoefu wao vina mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Waziri Masoud ameipongeza Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Diaspora Zanzibar kwa kuanzisha jukwaa huru la Diaspora, litakalokuwa sehemu ya kukusanya, kusikiliza na kujadili maoni na mapendekezo yao kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo. Amesisitiza umuhimu wa Diaspora kuendelea kuibua fursa mpya za maendeleo na kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo ushirikiano huo utasaidia kuimarisha uwekezaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Diaspora Zanzibar, Haji Gora, amesema jukwaa hilo litatoa nafasi kwa Diaspora kupaza sauti zao, kuwasilisha maoni na kueleza changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa ushirikiano na Serikali. Aidha, amesema ushirikiano kati ya Diaspora na Serikali ni muhimu katika kuitangaza Zanzibar kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuleta mawazo mapya yatakayochochea juhudi za kuimarisha maendeleo ya nchi.
