Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar - President's Office and Chairman of Revolutionary Council Diaspora

News and Events

MASHEHA WILAYA YA MJINI WAPATIWA ELIMU JUU KUWEPO KITENGO CHA DIASPORA ZANZIBAR


Mkuu wa Wilaya ya mjini ndugu Marina Joel Thomas akisoma hotuba ya ufunguzi wa semina ya kutoa elimu ya Mtengamano wa jumuia ya Afrika Mashariki na Diaspora kwa Masheha wa Wilaya Mjini iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari Kikwajuni.

Masheha katika Wilaya ya Mjini wametakiwa kuwa na utaratibu mzuri utakaohakikisha kwamba wanashirikiana vizuri na Wanadiaspora yaani wazanzibari wanaoishi nje ya nchi wakati wanapofika katika maeneo yao kwa lengo la kuratibu shughuli za utoaji wa misaada katika jamii zao.

Sheha wa Shehia ya Migombani nd.Msafiri Kitwana Msafiri kushoto pichani akiwa na masheha wenzake wakiwa katika semina hiyo.

Afisa wa Kitengo cha Diaspora Haji Ameir Haji akiwasilisha mada kwenye semina iliyowashirikisha masheha wa wilaya ya mjini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mjini ndugu Marina Joel Thomas wakati alipokuwa akizungumza na masheha wa Wilaya ya Mjini katika ufunguzi wa semina iliyolenga kutoa elimu ya kutoa mtangamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki na Diaspora iliyowashirikisha masheha wa Wilaya ya mjini katika ukumbi wa Baraza la zamani la wawakilishi Kikwajuni.
Alisema mchango wa wazanzibari walioko nje ya nchi unalenga kusaidia maendeleo katika jamii hivyo ni vyema kwa masheha wa Wilaya ya mjini kuufahamu vizuri mchango unaotolewa na wanadiaspora hao kwa kuithamini michango yao na kuwapa kila ushirikiano wakati wanapofika katika shehia zao.
Alisema jumuia za diaspora zilizoko nje ya nchi zinafahamika kisheria na zinalengo la kuisaidia jamii ambayo iko chini ya serikali za mitaa kupitia shehia zao.
Hivyo nd. Marina alielezea matumainio yake kwamba hatua ya kufanyika semina hiyo kwa masheha wa wilaya ya mjini kutaweza kutoa mtazamo mpya kwa masheha kutambua mchango wao kwa jumuia hizo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Semina hiyo ya siku mbili iliyowashirikisha zaidi ya masheha 45 kati ya masheha 52 wa wilaya ya mjini imeweza kujenga mwamko mpya kwa masheha hao kutambua dhana ya diasopora na umuhimu wake kwa Zanzibar.
Miongoni mwa mada zilizotolewa katika semina hiyo na kufanyiwa uchambuzi wa kina ni Diaspora na Maendeleo ya Zanzibar iliyowasilishwa na Afisa kutoka Idara ya Diaspora nd. Haji Ameir Haji. Uchambuzi wa mada hiyo ulianzia na utangulizi kwanini serikali iliamua kuanzisha Kitengo cha Uratibu wa Wazanzibari Wanaoishi Nchi za nje katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Pia masheha hao walipata fursa ya kutambua mikakati ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Diaspora ,Dhana ya Diaspora na kufahamu kwamba ni mtawanyiko wa watu wanaoishi nje ya mipaka ya nchi zao za asili ambao wamekwenda huko kuishi kwa sababu mbali mbali zikiwemo za kawaida na kwenda kufanyakazi.
Masheha hao wa Wilaya ya mjini pia walielezwa sera ya Diaspora Zanzibar jinsi ilivyolenga kuweka mazingira bora na rafiki yatakayowawezesha wanadiaspora kushiriki katika maendeleo ya Zanzibar. Majukumu ya Kitengo cha Diaspora nayo wameelezwa wazi katika semina hiyo kwamba pamoja na mambo mengine kitengo hicho kitaendelea kuwatafuta,kuwashajiisha na kuwashirikisha wanadiaspora ili waweze kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Tokea kuanzishwa kwa kitengo cha uratibu wa Wanadiaspora Zanzibar wamekuwa mstari wa mbele kuwekeza na kuanzisha miradi mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kuchangia katika sekta za afya na elimu ambapo maeneo kadhaa ya Unguja na Pemba yamefaidika na uwekezaji na misaada yao.
Mada nyengine iliyowasilishwa katika semina hiyo ni elimu inayohusiana na Mtangamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki na utekelezaji wa soko la pamoja iliyotolewa na Afisa wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Idara ya Diaspora Suleiman Muhsini.
Miongoni mwa mambo yaliyochambuliwa kwa kina ni pamoja na namna jumuia ya Afrika mashariki itaakavyoundwa, hatua zitakazopitiwa na itifaki ya soko la pamoja,Itifaki ya umoja wa sarafu na Itifaki ya kuanzisha Shirikisho la kisiasa la Jumuia ya Afrika Mashariki.
Fursa za Mtangamano wa Afrika Mashariki ni pamoja na fursa za kufanya biashara, fursa za kuwekeza(Uwekezaji),fursa za ajira,kasi ya uzalishaji,kutaangaza Biashara katika soko la Afrika Mashariki,fursa ya Wajasiriamali kujifunza,fursa la soko la viungo,fursa za kibiashara zitokanazo na nchi nyengine wananchama
Michango mingi ilitolewa na Masheha katika kuzichangia mada hizo na ushauri mkubwa ulitolewa na masheha wengi wa Wilaya ya Mjini wametaka kuwepo na uangaalizi wa kutosha katika usimamizi na utekelezaji wa masuala hayo muhimu ambayo yote ni msingi wa uhai na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
Semina hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi wa alielezea matumainio yake kwamba hatua ya kufanyika semina hiyo kwa masheha wa wilaya ya mjini kutaweza kutoa mwamko mpya kwa masheha kutambua mchango wao kwa jumuia hizo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii
Mkurugenzi Adila amewataka masheha hao kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi kwa kuwafikishia uelewa wa kuwepo dhana ya Diaspora kwa maendeleo ya Zanzibar.
Alisema Idara yake itakuwa inaziendeleza semina za aina hiyo katika ngazi za shehia, wanafunzi wa skuli za msingi,sekondari,vyuo, wabunge pamoja na wawakilishi zote zikiwa na lengo la kutoa elimu ya Diaspora.
Mkurugenzi huyo amewapongeza wazanzibari walioko nje ya nchi ambao wameitikia wito wa serikali kwa kuanzisha jumuia hizo ambazo tayari zimeshaanza kusaidia harakati mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

  • Google+
  • PrintFriendly