Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar - President's Office and Chairman of Revolutionary Council Diaspora

News and Events

Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Diaspora Yazungumza na Wanadiaspora.


Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na uratibu wa Diaspora Zanzibar ilikutana na wajumbe na wawakilishi wa Jumuiya mbalimbali za Wazanzibari wanaoishi Nje ya Nchi (Diaspora) kwa lengo la kujadili namna nzuri ya kuimarisha mashirikiano baina ya Wazanzibari wanaoishi Nchi za Nje na Idara ya uratibu wa masuala ya Diaspora Zanzibar ili kufanikisha adhma ya Serikali ya kujenga mazingira mazuri na rafiki yatakayo rahisisha ushirikishwaji wa Diaspora katika ajenda ya maendeleo ya nchi yao.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 26 Oktoba, 2017 katika ukumbi wa ofisi hiyo uliyopo Vuga Zanzibar, kiliongozwa na Ndg. Rahma Ali Khamis ambae ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (ORMBLM).

Wajumbe wa kikao hicho walipata nafasi ya kujadili mambo mbalimbali yanayolenga namna ya kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wanadiaspora hao kupitia jumuiya zao, miongoni mwa masuala yaliyojitokeza katika majadiliano hayo ni:-

a. Kurahisisha upatikanaji wa vibali vya ukaazi na vibali vya kazi (Resident and Work Permit) kwa wanadiaspora ambao wameamua kurudi ama kuchangia walichonacho katika kuiendeleza nchi yao.

b. Kuimarisha mawasiliano (Networking) baina ya Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje ya Nchi na wanadiaspora wenyewe ili kukuza maelewano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jumuiya za wanadiaspora kote ulimwenguni jambo ambalo litarahisisha na kuchapuza kasi ya maendeleo kupitia wanadiaspora.

c.  Ajenda ya Uraia Pacha “Dual Citizenship”, wajumbe walipendekeza ajenda ya uraia pacha itolewe elimu kwa wananchi na uongozi wa serikali ili kuwashawishi kulikubali suala hilo hata katika siku za baadae kwa kuwa ni jambo muhimu sana kwa kuwa linatoa fursa kubwa zaidi kwa wanadiaspora kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.

d. Utoaji wa Vitambulisho kwa Wanadiaspora wa Zanzibar. Wajumbe walionesha haja na shauku yao ya kupatiwa vitambulisho ambavyo wanaamini itakuwa ni suluhisho na kuondoa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wanapoamua kujitoa na kuchangia maendeleo ya nchi yetu.

e. Ufanyaji wa utafiti na upangaji wa mkakati wa kitaalamu wa utatuzi wa changamoto za maendeleo. Wajumbe walihimizwa kufanya utafiti wa kina ili kugundua fursa na changamoto zilizopo katika jamii na kuwa na uelewa mzuri wa kushughulikia changamoto hizo jambo ambalo litafanya michango na misaada inayotolewa kutumika ipasavyo kwa walengwa.

Licha ya changamoto nyingi zilizopo katika ushirikishwaji wa wanadiaspora wa Zanzibar katika ajenda ya maendeleo ya nchi yao, bado kuna mambo mingi ya kujivunia kwa uwepo wa wazanzibari hao kwani hadi hivi sasa wameshachangia misaada ya hali na mali katika sekta za elimu na afya ambazo ndio sekta zilizotiliwa mkazo kwani ndio roho ya taifa, lakini pia kupitia kikao hicho waliombwa wajaribu kutafuta namna nzuri ya kuchangia ikiwemo kuhaulisha ujuzi na teknolojia wanazozipata huko wanakoishi.

  • Google+
  • PrintFriendly